ZIJUE MBINU ZA KUWA MJASIRIAMALI.
Uchumi wa Tanzania umekuwa ukizalisha ajira chache kila siku. Hii imekuwa ikifanya vijana wengi wanaohitimu vyuoni kubaki wakizunguka na bahasha kila kona kusaka ajira.
Takwimu kutoka ofisi ya takwimu ya taifa zinaonyesha kuwa mwaka 2014 taifa lilizalisha nafasi za ajira 282,382 tu ukilinganisha na mahitaji ya zaidi ya wahitimu 400,000 wanaomaliza vyuo kila mwaka.
Hii inaonyesha dhahiri kuwa Tanzania kama nchi inahitaji kuweka nguvu za ziada katika kuhakikisha kuwa nafasi zaidi za ajira zinatengenezwa.
Pengine njia pekee inayoweza kutumiwa kupunguza tatizo hili au hata kulimaliza kabisa ni kupitia ajira binafsi (Ujasiriamali).
Pamoja na kuwa ujasiriamali unaweza kuwa suluhisho la ajira nchini, vijana wengi wameshindwa kabisa kufanya ujasiriamali kutokana na kukosa elimu sahihi. Kwa bahati mbaya sana mfumo wetu wa elimu haumsaidii sana muhitimu kupata stadi za ujasiriamali.
Katika vipaumbele vyake, Rais John Magufuli anasisitiza sana Tanzania ya viwanda, lakini hili litatokea tu kama vijana wa kitanzania watapatiwa elimu ya ujasiriamali.
Sehemu hii itakuwa ikiwapatia makala mbalimbali za ujasiriamali… tutajifunza jinsi ya kuanzisha biashara, jinsi ya kuendeleza biashara yako na namna ya kupata fedha.
Leo tutaanza kujifunza mambo ya msingi katika kuanzisha biashara.
Mambo ya Msingi katika kuanzisha biashara
Biashara yoyote huanza na wazo, ila wazo pekee halitoshi, linahitaji kufanyiwa kazi. Hapo ndipo watu wengi huweza kuanza kujisikia kuzidiwa. Si ajabu kuona mtu anakatishwa tamaa kwa kutizama msururu wa mambo yanayohitajika ili kuanzisha biashara, lakini pia kuanzisha biashara ni rahisi kuliko unavyodhani. Kama ilivyo katika lengo lolote kubwa, ukianza kwa kutengeneza malengo madogo madogo ya kutekeleza utaweza kufanya mambo yote muhimu katika kuanzisha biashara.
Jinsi ya Kuanzisha Biashara Ndogo
Kuanzisha na kuendesha biashara inahitaji msukumo, nia na kipaji. Inahitaji pia utafiti na mipango. Kama ilivyo kwenye mchezo wa drafti, mafanikio kwenye biashara ndogo huanza na maamuzi sahihi katika hatua za mwanzoni. Ikumbukwe pia hapa kuwa pamoja na kwamba makosa madogomadogo ya mwanzoni yanaweza yasiue biashara yako, inahitaji ujuzi, nidhamu, na bidii kuyasahihisha.
Ili kuboresha uwezekano wa kufanikiwa, unapaswa kutenga muda wa kujichunguza na kutathmini malengo yako kibiashara na malengo binafsi. Tumia taarifa hiyo kutengeneza kwa umakini mkubwa mpango wa biashara ambao utakuwezesha kufikia malengo yako.
Mchakato wa kuandaa mchanganuo wa biashara utakuchochea kufikiria hata baadhi ya mambo ambayo usingekumbuka kuyafikiria katika hali ya kawaida. Mchanganuo wako utakuwa zana muhimu sana unapopambana kutafuta fedha kwa ajili ya biashara yako. Mchanganuo huo pia unaweza kutumika kama kigezo cha kila mara kufuatilia/ kupima mafanikio ya biashara yako.
Yako mambo kadhaa yanayohitajika katika biashara yoyote.
Jambo la kwanza kabla ya kuanzisha biashara ni kuwa unatakiwa ujiulize sababu za wewe kutaka kuingia kwenye biashara. Sababu zilizozoeleka za kuanza biashara ni:
Unataka kujiongoza mwenyewe.
Unataka uhuru wa kifedha.
Unataka uhuru wa kutumia ubunifu wako.
Unataka kutumia kikamilifu ujuzi na ufahamu wako
Jambo la pili ni kuamua biashara ipi inakufaa? Ili kufahamu ni biashara ipi inakufaa, jiulize maswali yafuatayo:
Ninapenda kutumiaje muda wangu?
Nimejifunza au kusomea ujuzi gani?
Watu wengine wanazungumzia ubora wangu kwenye mambo gani?
Nina muda kiasi gani kuendesha biashara kwa ufanisi?
Katika mambo ninayopendelea yapo ambayo yanaweza yakawa fursa ya biashara?
Biashara yangu itahudumia sehemu/ kundi gani katika soko?
Je? Wazo langu linatekelezeka na litakidhi hitaji katika soko?
Ushindani nilionao ni upi? Nami nina uwezo gani katika ushindani?
Biashara yangu ina manufaa gani kuzidi zingine zilizopo?
Je? Naweza kutoa huduma zenye ubora zaidi?
Je? Naweza kutafuta soko kwa ajili ya bidhaa/ huduma zangu?
Ukishapata majibu ya maswali hayo hapo juu ni wazi kuwa utakuwa ulishaanza kujua ni biashara gani unaweza kuianzisha. Lakini pia unatakiwa ujiulize maswali haya hapa ili kuwa na uhakika na biashara ambayo
Leave a Comment